Jumamosi , 19th Mei , 2018

Msanii wa Bongo Fleva ambaye anafanya vizuri na kibao chake kipya cha 'Mvumo wa Radi' Ali Saleh Gentamilan maarufu kama Alikiba amefunguka na kudai tayari ameshamaliza kutengeneza albamu yake ya muziki na muda wowote anaweza kuiachia rasmi.

Alikiba amebainisha hayo wakati alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha Planet Bongo ndani ya Heshima ya BongoFleva inayorushwa mubashara kupitia EATV na kusema anayo mipango ya kuwapa mashabiki zake albamu kama wanavyofanya baadhi ya wasanii kwa sasa.

"Mpango wa albamu upo na labda niseme tu, nipo nayo tayari ila bado kuiachia. Kwasababu kuna kipindi ambacho tulikuwa tunaona kuuza single kuna pesa zaidi ya albamu kutokana na albamu ilikuwa haina faida kwa maana ukiachia nyimbo 8 au 10 mtu anakuwa anasikiliza hizo hizo kila siku na hata ukitoa nyimbo nyingine hawezi kusikiliza", amesema Alikiba.

Alikiba alifanikiwa kutoa albamu yake ya kwanza mwaka 2007 aliyoipa jina la 'Cinderela' ambayo ilikuwa ni kati ya albamu bora na iliyouza zaidi mwaka huo Afrika Mashariki. Mwaka 2008 Alikiba aliachia albamu yake ya Pili 'Alikiba 4 Real' ambayo nayo pia ilifanya vizuri sokoni na kumpa Tuzo mbalimbali.