Alhamisi , 3rd Oct , 2019

Mchekeshaji wa muda mrefu nchini Tanzania maarufu kwa jina la Pembe,amesema kuwa uhalisi wa maisha ya watu wengi waishio vijijini, wanaotumia silaha za jadi katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku, ndicho kilichomvutia na yeye kuoneka na rungu katika filamu zake zote.

Akizungumza na EATV & EA Radio Digital, kuhusu kutembea na rungu kwa muda mrefu amesema, anafanya hivyo ili kuweka uhalisia wa maisha ya vijijini, ambapo aligusia baadhi ya vijana wanaotokea Kondoa pamoja na wamasai wenye utamaduni wa kutembea na mapanga kiunoni.

Kila mtu anataka kuigiza jinsi matajiri walivyo, Je hawa maskini wa vijijini na mafukara atawasemea nani, Mimi napenda kuigiza kuhusu kuwa mapepe na mcharuko ndiyo 'style' yangu pia nawawakilisha watu wa aina hiyo siwezi kung'ang'ania kuigiza kama mtu wa maghorofa au suti,siri ya lile rungu ni mizizi ambayo wenyewe wanajua maana yake hata mimi nilinunua tu sijui linatokea wapi” amesema Pembe.

Aidha Pembe ameongeza kuwa yeye na rafiki yake Senga, hawana akaunti za mitandao ya kijamii ila kuna watu feki, wanaotumia majina yao na picha zao ili kuwachafua kwa kuchapisha vitu visivyo na maana na uongo dhidi yao.