Ijumaa , 23rd Mar , 2018

Msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye pia kwa sasa ni mbunge Profesa Jay, amefunguka juu ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kufungia wasanii na baadhi ya kazi zao, na kusema kuwa suala hilo sio sahihi.

Akizungumza na www.eatv.tv, Prof Jay amesema BASATA wanapaswa kukaa na wasanii na kuzungumza nao, ikiwezekana kutoa semina elekezi, lakini sio kuwafungia kwani wasanii wanapitia mengi magumu kwenye kutengeneza kazi zao.

Prof. Jay amesema kwamba serikali inafahamu kubwa ya jamii ni vijana, na wengi wao wanajishughulisha na sanaa ili kujipatia kipato, wanapofanya hivyo wanawakwamisha vijana hao ambao wanapigana kujitoa kimaisha..

“Unajua asilimia kubwa ya taifa ni vijana, na wengi wao wanajishughulisha na sanaa mbali mbali, suala la kufunginwa huu mziki tumetoka nao mbali sana, mtoto akikosea usimchinje kichwa, tujaribu kufanya semina elekezi, kumfungia mtu kama roma ni kitu kikubwa, hii inarudisha nyuma na inakatisa tamaa”, amesema Prof. Jay.

Prof Jay ameendelea kwa kusema kwamba yeye kama muwakilishi wa wananchi na wasanii pia, atalisemea hili bila kuchoka.