Ijumaa , 18th Dec , 2015

Mama mzazi wa msanii Hisia ambaye pia alikuwa mgombea wa kiti cha Urais kupitia chama cha ACT Wazalendo Bi. Anna Mghwira, amesema pamoja na kijana wake huyo kufanya muziki, wanatofautiana katika muziki wake.

Anna Mghwira ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kuwa kitendo cha kuandika nyimbo zenye maudhui ya mapenzi, na yeye akitamani mtoto wake huyo atunge nyimbo zenye ujumbe unaolenga jamii ndipo wanapotofautiana.

“Kwanza hapo tunatofautiana mi na yeye kwamba anapenda kuimba nyimbo za mapenzi, mimi sina interest kwanza sionagi kitu kipya kwenye hayo mambo, ye ananiambiaga labda wewe umezeeka, lakini natamani sana aimbe mambo ya maisha zaidi, anapenda kuimba nyimbo za solo, solo nyingi huwa ni mapenzi, sijaona solo ihamishwe ipelewe kwenye mazingira, maji, elimu, ukimwi na vitu vya namna hiyo, vitu ambavyo mimi ningependa mtu aimbe”, alisema Anna Mghwira.

Akizungumzia kipaji cha mtoto wake huyo Anna Mghwira alisema Hisia amepata kipaji hicho toka kwake, kwani kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa anaimba, na kuelezea sababu za mtoto wake huyo kutoonyesha kumsapoti wakati wa kampeni, kama wasanii wengine walivyokuwa wanafanya kwa baadhi ya wagombea wa Urais hapa nchini.

“Mimi binafsi sikuona sababu ya kukatisha mtoto masomo, alafu wasanii wako wengi kama ningetaka kutumia, mi sikutumia msanii, kwa hiyo kama sikutumia wasanii wowote nisingemtumia yeye kunibeba beba tu mimi, kwanza haikuwepo kwenye utaratibu wetu na binafsi sijui kama ningetaka”, alisema Anna Mghwira.

Msanii wa Bongo Fleva Hisia ambaye ndiye mtoto wa mama Anna Mghwira.