Ijumaa , 17th Aug , 2018

Msanii wa filamu bongo, Daudi Michael maarufu kama 'Duma' amedai wasanii wengi wameshindwa kuendelea kuishi katika soko la filamu nchini kutokana na kuzoea kupewa fedha na baadhi ya wasambaji ili kusudi waweze kufanya kazi waliotumwa jambo ambalo kwa sasa watu hao hawafanyi tena.

Msanii wa filamu bongo, Daudi Michael maarufu kama 'Duma'

Duma amebainisha hayo wakati alipokuwa anazungumza na www.eatv.tv baada ya kuwepo wimbi kubwa la wasanii kupungua katika soko la filamu, jambo ambalo wafuatiliaji na wapenzi wa tasnia hiyo kudai huenda bongo movie imekufa au kutolipa katika nyakati hizi. 

"Ninapambana na nitaendelea kufanya hivyo hadi tone langu la mwisho, ili kusudi soko la filamu liweze kurudi kwenye 'chart' yake kama ilivyokuwa hapo awali. Sitoweza kukubali kushindwa katika hili", amesema Duma.

Mbali na hilo, Duma amefafanua baadhi ya mambo kuwa kinachowafanya wasanii wengi wa filamu kushindwa kutoa kazi zao kama ilivyokuwa hapo awali ni kutokana na ma-boss waliokuwa wanawapa fedha, sasa hawatoi tena.

"Ma-boss hawatoi fedha tena sasa hivi kutokana kutosheka na movie walizokuwa nazo,  wasanii waliowengi hawamiliki filamu za kwao binafsi bali wao wanakuwa kama vibarua tu wa kufanyakazi kutokana na bajeti walizopewa na watu hao", amesisitiza Duma.

Kwa upande mwingine, Duma anatarajia kuachia kazi yake mpya kesho inayokwenda kwa jina la 'nipe changu', ambayo imejumuisha wasanii mbalimbali pamoja na kuwa na maudhui ya kitofauti na jinsi watanzania walivyozoea kuzitazama.