Alhamisi , 16th Aug , 2018

Msanii wa filamu nchini, Jennifer Kyaka, maarufu kama 'Odama' amefunguka na kuwataka Watanzania kuacha kuishi na vinyongo moyoni mwao, na badala yake wanapaswa kuzungumza moja kwa moja na muhusika wa jambo linalowakwaza ili kulipatia ufumbuzi.

Msanii wa filamu nchini, Jennifer Kyaka, maarufu kama 'Odama'

Odama ametoa kauli hiyo leo asubuhi, wakati alipokuwa anazungumza na tofuti ya www.eatv.tv ikiwa imepita siku moja tangu msanii huyo kuzushiwa taarifa ya kifo kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii hadi mwisho wa siku kumfikia yeye mwenyewe taarifa hizo.

"Hakuna sababu ya kuendelea kuishi na vinyongo, kwa sababu mtu kama huyo aliyenitendea mimi huo ubaya anaishi na kinyongo. Pia hakuna sababu za msingi za kuombeana kifo licha ya kuwa binadamu sote tutakufa kwa nyakati zilizopangwa. Sijaenda kushtaki popote pale hadi dakiki hii ila ninajua kitu gani nitafanya kuhusiana na mtu huyo," amesema Odama.

Pamoja na hayo, Odama ameendelea na kusema "nashindwa kuelewa ni kwanini huyo mtu amenifanyia hivyo kwa sababu sina kumbukumbu ya ugomvi na mtu yeyote yule ambao upo 'serious' kiasi hicho. Kiukweli kwa mara ya kwanza nilipoiona hiyo taarifa ya kifo kwenye 'group' za 'Whatsapp' niliishiwa nguvu kabisa, hata ya kuendesha gari nikashindwa na nikaegesha pembeni yaani siwezi kuelezea hisia zilizokuwa zimenijia wakati huo".

Hii ni mara ya kwanza kwa muigizaji Odama kuzushiwa kwamba amefariki dunia kwenye mitandao ya kijamii hadi kupelekea kuchanganya watu wake wa karibu, marafiki, ndugu na mashabiki zake mbalimbali wanaofuatilia kazi zake za sanaa.

Msikilize hapa chini Odama mwenye kwa kauli yake akielezea kwa kina jinsi alivyopokea taarifa hiyo ya msiba wake wakati yeye mwenye bado akiwa hai akidunda na kupumua vyema hewa ya muumba.