Z Anto amuimbia Lissu

Sunday , 10th Sep , 2017

Msanii Z Anto amefunguka na kudai ameguswa na tukio lilimpata Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu la kupigwa risasi na watu wasiofahamika hivyo ameamua kuachia nyimbo kwa lengo la kuwakumbusha watanzania kudumisha amani pamoja na kumuombea Lissu

Z Anto amebainisha hayo wakati akifanya mahojiano maalum na mwandishi wa EATV baada ya kupita muda mchache alipoachia wimbo wake uliopewa jina la tumuombee Lissu. 

"Nimeguswa sana na hili suala la Mhe. Tundu Lissu na nikiwa kama mzalendo ninayeitakia mema nchi yangu nimeona ni bora nitoe nyimbo kwa ajili ya kuwakumbusha na kuwasisitiza watanzania wenzangu tuendelea kumuombea dua Mhe. Lissu", amesema Z Anto.

Pamoja na hayo, Z Anto ameendelea kwa kusema "ikiwa wabunge kwa pamoja waliweza kutoa nusu ya posho zao za kikao cha siku kimoja kuweza kumsaidia Lissu kwa ajili ya matibabu nami kwa upande wangu nikaona siyo vibaya kutoa nyimbo kama sehemu ya mchango kwake ili kwa pamoja watanzania tuungane kumuombea dua kwa sababu tukio lilimtokea siyo la kawaida.  Huu wimbo siyo wa kisiasa wala chama fulani ila ni wa kila mtanzania", amesisitizia Z Anto.

Kwa upande mwingine, Z Anto amewataka wasanii wenzake  wawe na moyo wa uzalendo kwanza ili kuweza kudumisha na kutangaza amani ya nchi.

Kama hujapata bahati ya kusikiliza wimbo huo bonyeza hapa chini kusikia alichokiimba Z Anto kuhusu Mhe. Tundu Lissu