Ajiua kwa kunyimwa pesa na mkewe

Jumatatu , 3rd Jun , 2019

James Kamau mwenye miaka 39 mkazi wa kijiji cha Mbogo-ini kilichoko katika kata ya Kahumbu kaunti ya Murang'a nchini Kenya, amejiua baada ya kunyimwa pesa ya kwenda kunywa pombe na mke wake .

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa Murang’a, Josephat Kinyua amesema kwamba mwanaume huyo baada ya kutoka kwenye shughuli za kila siku alizokuwa akizifanya, alipitia bar na rafiki yake na kuanza kunywa pombe huku yeye akiwa mlipaji, lakini alipomaliza pesa alirudi nyumbani na kutaka mkewe ampatie pesa nyingine.

“Inaarifiwa kuwa Bw. Kamau alirejea nyumbani kwao ambapo watoto wao watatu walikuwa usingizini, alizua fujo akitaka apewe pesa kwa lazima, baada ya mama yake kusikia vurugu hizo, alimchukua mke wa Kamau na kumpa malazi", amesema Kamanda Kinyua

"Kwa hasira, Kamau alisikika akimuonya mama yake kuwa alikuwa na upendeleo kwa mkewe na akaapa kuwaadhibu wote wawili kwa maombolezi kisha akafunga mlango.  Asubuhi yake watoto walipoamka, wakamwona baba yao akining’inia kutoka kwa paa la nyumba sebuleni, ameongeza Kamanda.

Taarifa zaidi zinasema kwamba baada ya tukio hilo walitoa taarifa polisi, na kukuta tayari mtu huyo ameshafariki, na kuchukua mwili kwenda kuuhifadhi katika hospitali ya Murang’a.