Jumanne , 24th Sep , 2019

Mkazi wa Kawe kwa Mzimuni Jijini Dar es Salaam, Bi. Mariam Augustino amepoteza uwezo wake wa kuona kwa muda wa miaka mitatu, ikiwa ni katika harakati za kupigania mirathi ya marehemu mume wake.

Bi Mariam amesema kuwa migogoro ya kifamilia imezuka mara baada ya mumewe kufariki takribani miaka mitatu iliyopita, ambayo imepelekea kupata presha ya macho anayopambana nayo hadi sasa akiwa haoni.

Akizungumza na EATV & EA Radio Digital, Bi Mariam ameeleza jinsi ndugu wa upande wa marehemu mume wake wanavyosababisha usumbufu dhidi yake mara kwa mara, wakimtaka asijihusishe na chochote kinachohusiana na nyumba hiyo licha ya yeye kuwa na hati zote  zinazothibitisha uhalali wa kumiliki na kulipia kodi ya ardhi na jengo mara zote zinapohitajika.

''Familia haikunitendea haki, mimi nilitafuta mali na mume wangu nikatengeneza lakini walijaribu kunipeleka mahakamani na kesi nikashinda. Pamoja na kushinda kesi familia ikaja juu kudai kwamba mali za kwao, kila ninapojitahidi msaada sipati wao wapo wengi na mimi nipo peke yangu", amesema Bi Mariam.

Nae kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mzimuni Kawe, Hassan Ngonyani ameeleza kwamba mgogogoro uliopo baina ya pande hizo mbili ni wa kimaslahi, ambapo upande mmoja wa familia una umiliki halali wa kiwanja na upande mwingine una umiliki halali wa nyumba.

''Wadogo zake marehemu na wanafamilia wanamwambia kama anataka nyumba yake aitoe katika kiwanja hicho lakini wamekiri kuwa mchango mkubwa wa kujenga nyumba hiyo ulitoka kwa ndugu yao lakini kwa makubaliano ya baba yake ambaye pia ndiye baba yao wao '', ameeleza Hassan Ngonyani.

Aidha Bi.Mariam ameomba msaada kwa Watanzania kufuatilia suala hilo kwani mtu anayemtegemea hivi sasa ni mmoja tu ambaye ni mtoto wake wa kwanza.