Ijumaa , 21st Sep , 2018

Mkazo (Stress) ni hali ya mwili au akili ya mwanadamu kuitikia mahitaji mbalimbali, ambayo husababishwa na matukio mazuri au mabaya yanayomtokea katika shughuli zake za kila siku.

Kiafya mtu anapopata mkazo wa kitu chochote kinachomzunguka, mwili wake huitikia kwa kuzalisha kemikali ambayo huingia katika damu, ambayo baadaye huzalisha nguvu inayoweza kumsaidia endapo mkazo huo utakuwa umetokana na hatari fulani. Lakini nguvu hiyo inaweza kuwa na madhara mwilini endapo itakuwa imetokana na mkazo wa hisia na kusiwe na sehemu ambayo inaweza kutumika.

Hizi ni njia tano zinazoweza kukusaidia kuepukana au kuondoa mkazo (Stress) mwilini.

Kuepuka matumizi ya pombe na Sigara, matumizi ya muda mrefu ya vitu hivi yanaweza kusababisha mkazo kuongezeka mwilini badala ya kupunguza, kutokana na kuwepo kwa kemikali mbalimbali kama (alcohol) kwenye pombe na (nicotine) inayopatikana kwenye sigara, ambazo zinaongeza tatizo hilo.

Pata muda wa kutosha wa kulala, kukosa usingizi kunaweza kusababisha mkazo mwilini japo pia wakati mwingine mkazo unaweza ukasababisha tatizo la kukosa usingizi. Badala ya kutumia madawa ya kupunguza maumivu, inashauriwa mtu apate muda mwingi wa kupumzika na kulala ikiwemo kutojihusisha na kazi zinazohitaji akili zaidi masaa machache kabla ya kulala na kusoma katika mazingira tulivu.

Fanya mazungumzo na watu wa karibu, mazungumzo yanamfanya mtu kuipumzisha akili na kusahau matatizo na vitu vinavyomsababishia mkazo, inashauriwa mtu anapohisi tatizo hilo ajitahidi kuzungumza kwa lugha rahisi na watu wake wa karibu, wafanyakazi wenzake, marafiki na washauri wake wa masuala mbalimbali kuhusiana na njia sahihi za kuepuka tatizo hilo.

Tumia vizuri muda wako, mara nyingi tumekuwa tukijikuta na mzigo mkubwa wa kutokamilisha kazi tulizojipangia. Jambo hilo linaweza kusababisha mkazo endapo halitopangiliwa vizuri, inashauriwa kuwa na ratiba nzuri ya vitu vya kufanya kutokana na muda maalum kutoka vitu vidogo, vya kati hadi vikubwa ambavyo vinahitaji muda mrefu.

Jifunze kutatua changamoto zako, mkazo pia unaweza kusababishwa na uwoga wa matatizo ambayo mtu anakabiliwa nayo, ni pale mtu anapoliona tatizo alilonalo kuwa ni kubwa na lisiloweza kutatulika. Moja kati ya njia nzuri ya kutatua matatizo ni kuyaorodhesha kisha kuja na mbadala wa utatuzi wake kadri vile mtu anavyoweza, ikiwemo kuorodhesha hatua mbalimbali za utatuzi wa tatizo, mfano, kipi kinahitajika kufanyika, kitafanyika vipi, wakati gani, wapi na nani atahusika.