Kibonde azikwa leo, wasanii waaswa kuacha majivuno

Jumamosi , 9th Mar , 2019

Aliyekuwa mtangazaji wa Clouds Media Group (CMG), Ephraim Kibonde, amezikwa leo katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, sehemu ambayo alizikwa mke wake, Sarah, aliyefariki dunia Julai, mwaka jana.

Jeneza lenye mwili wa marehemu Ephrahim Kibonde.

Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi mkurugenzi mtendaji wa Clouds Media, Joseph Kusaga amewasihi watu maarufu hasa wasanii kuishi kwa upendo na kutowekeana chuki, kwakile alichodai kuwa kifo hakitazami umaarufu wala utajiri.

"Sisi Vijana tuache nyodo, tupendane, Mungu anaweza kukuchukua wakati wowote, kama ni umaarufu Ruge alikuwa nao kuliko wasanii wote na Kibonde alikuwa nao kuliko wasanii wote lakini leo hatuko nao", amesema Kusaga.

Kibonde alifariki dunia juzi jijini Mwanza kwa shinikizo la damu wakati jitihada za kumhamishia Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Bugando kutoka Hospitali ya Uhuru zikifanyika.

Kibonde alianza kujisikia vibaya kabla ya kuzikwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa CMG, Ruge Mutahaba, Bukoba mkoani Kagera na kupelekwa Hospitali ya rufani ya Mkoa wa Kagera ya Bukoba na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Uhuru.