Mafuriko yaua 28, Rais atoa maagizo

Jumanne , 12th Mar , 2019

Watu 28 wamepoteza maisha kutokana na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko Kusini mwa nchi Malawi, ambapo taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo iliyotolewa imesema kuwa idadi ya walioathirika inatarajia kuongezeka.

Sehemu ya mafuriko nchini Malawi.

Msemaji wa Wizara hiyo anayehusika na udhibiti wa maafa, Chipiliro Khamula, amesema watu 124 wamejeruhiwa huku takribani wengine zaidi ya 200,000 wamelazimika kuhama makazi yao katika jumla ya wilaya 14.

Wakati huohuo Rais wa Malawi, Arthur Peter Mutharika ametangaza tukio hilo kuwa janga la kitaifa baada ya dhoruba kali kusababisha kuta za mito kubomoka na mafuriko kufunika vijiji hivyo.

Katika maeneo hayo umeme umekatika na huduma ya maji imekosekana, Rais Mutharika ameelekeza misaada ya dharura kupelekwa katika maeneo hayo yaliyoathirika na kuratibiwa kwa haraka huku akilitaka Jeshi la Malawi kusaidia katika zoezi la uokoaji.

Dhoruba hiyo pia imesababisha mafuriko katika baadhi ya mikoa nchini Msumbiji.

Bofya link hapo chini.