Alhamisi , 4th Oct , 2018

Polisi katika eneo la Rukiga nchini Uganda, wamewashikilia wanawake 7 na mchungaji wao, kwa kusali wakiwa watupu ndani ya nyumba ambayo wao wamedai kuwa ndio kanisa lao.

Watu hao ambao wamedai ni waumini wa kanisa la Full Gospel wamekutwa kwenye nyumba ya mmoja wao anayejulikana kwa jina la Adah Kahababo, huko Rukiga.

Akizungumzia kukamatwa kwao Kamishna wa makazi wa wilaya Emmy Ngabirano na Mkuu wa Polisi wa eneo hilo, wamesema kwamba watu hao ambao ni wake za watu, wameshangazwa na kitendo hicho, ambacho licha ya kuvunja maadili, pia ni jambo la kushangaza.

“Tunaheshimu uhuru wa kuabudu, lakini watu lazima wafuate utaratibu wa kuendesha kanisa, watu waliokamatwa walikuwa wanaendesha kusanyiko kinyume na sheria, tena ndani ya nyumba ya mtu ambayo wamedai ni kanisa lao, sisi kama watu wa usalama hatuwezi kuliacha kwa sababu mwaka 2000 kuna watu walichomwa moto kanisani kwa tukio kama hili”, amesema Kamishna Ngabirano.

Hata hivyo waume wa wanawake hao wamesema wake zao wameyakimbia makazi yao kwa takriban wiki mpaka sasa, na kwenda kuweka kambi kwa Bi. Kahabado kwa ajili ya maombi ya usiku na mchana.

Waliokamatwa ni Mch. Agrey Elias Mubangizi, Adah Kahabado, Christina Arinda, Hope Nyamurungi, Apohia Tumusiime, Anna Mugabirwe, Angela Nyangoma na Moreen Nyangoma.