Mpenzi wa Chidi Benz aeleza alivyoitumia "unga"

Alhamisi , 23rd Jan , 2020

Kipindi cha Planet Bongo ya East Africa Radio, kinachoruka siku za wiki kuanzia 7:00 mchana hadi saa 10:00 jioni, kimepiga stori na mama watoto wa msanii Chidi Benz aitwaye Mariam, na ameeleza jinsi alivyoingia kwenye utumiaji wa madawa ya kulevya.

Msanii Chidi Benz na mzazi mwenziye Mariam

Mariam amesema alianza kutumia madawa ya kulevya aina ya Heroine, wakati yupo kwenye mahusiano na mwanaume mwingine kabla ya kuwa na Chidi Benz, ambaye wamejaliwa kupata watoto wawili.

"Kila mtu anasababu zake ila wengi wao kinachosababisha waingie huko ni makundi tu, kama mshikaji wangu anatumia na yeye atumie hata mimi kwa mara ya kwanza navuta madawa sikujua kama nimeingia huko, ila nilikuwa navuta sigara ikawa rahisi mimi kuvuta unga" amesema mzazi mwenza wa Chidi Benz.

Aidha ameendelea kusema "Hakuwa Chidi Benz aliyeniingiza kwenye madawa, nilikuwa na mwanaume mwingine kabla sijakutana na Chidi Benz, sikujijua kama navuta unga ila nilikuwa nahisi kitu kingine na hakuwahi kuniambia kama inapatikana wapi, unachukua tumbaku inanyongwa upya halafu unachukua unga unausaga kisha unaukwangua na kiwembe" ameongeza.