Alhamisi , 7th Feb , 2019

Tarehe 6 Februari ya kila mwaka ni siku ya kupinga vita dhidi ya ukeketaji duniani, ambapo iliridhiwa na Baraza la Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza mwaka 2003.

moja ya hatua za ukeketaji

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya wanawake milioni 200 wamekeketwa mpaka sasa, wengi kati yao ambao ni karibia nusu wakipatikana katika nchi za Misri, Ethipia na Indonesia.

Katika kuiadhimisha siku hiyo ambayo imeadhimishwa kitaifa Mkoani Mara, mama mmoja aitwaye Prisca Magesa katika kipindi cha Mjadala cha EATV saa 1, ameelezea hali yake halisi ya kimahusiano anayopitia katika maisha yake licha ya kuwa ameshazaa watoto watano hivi sasa.

Mama huyo amesema aliolewa akiwa na miaka 14 na mwanaume mwenye umri wa miaka 70, ambapo kabla ya kuolewa alikuwa akimsaidia mama yake kufanya kazi ya ukeketaji, hali iliyopelekea na yeye kufanyiwa kitendo hicho.

Pia amezungumzia namna ambavyo anaumia pale wanawake wenzake wanapokuwa wakizungumzia juu ya raha wanayoiptaka katika tendo la ndoa ilhali yeye hahisi raha yoyote anapokutana na mwanaume katika kipindi chote alichoishi na hali hiyo.

"Kwa upande wangu mimi kwanza huwezi kujisikia raha kwenye tendo la ndoa, yaani upoupo tuu, pia unapokuwa na wanawake wenzako wa makabila tofauti na wewe, wanapoongea madhara yake unajisikia kama umetengwa na mpweke", amesema Prisca.

Mtazame hapa akielezea zaidi.