Unataka kuwa mjasiriamali mzuri?, soma hapa

Jumapili , 7th Oct , 2018

Siku zote maamuzi ya kuanzisha safari ya ujasiriamali huwa ni magumu kwa walio wengi, hakuna dhamana yoyote ili kuyafikia mafanikio ya safari hii na hakuna njia yoyote itakayokuonesha kwamba sasa uko tayari kukabiliana na changamoto utakazokutana nazo katika safari yako.

Licha ya changamoto zote zilizopo katika ujasiriamali, endapo ukipata kitu kizuri cha kufanya, kitakupa mafanikio makubwa ambayo yanaweza kubadilisha maisha yako yote. Zingatia vitu hivi vitano, kabla hujafikiria kuanzisha biashara yoyote.

Geuza wazo kuwa mpango

Kila biashara inayonzishwa basi tambua ilianza kuwa wazo, lakini ni namna gani utaligeuza wazo kuwa uhalisia?. Tenga muda wako wa kuandaa mpango kazi wa wazo lako pamoja na changamoto utakazokutana nazo katika mpango kazi huo, kwa kufanya hivyo itakusaidia kutambua urahisi au ugumu wa kitu unachotaka kukifanya.

Kuwa na nidhamu

Hiki ndicho kitu kikubwa sana kitakachosaidia kuendesha mpango kazi wako, tambua kuwa wewe ndiye moyo wa biashara yako kwa maana kwamba wewe ndiye utakayeshikilia majukumu yote ya kiuendeshaji. Kama mjasiriamali, tambua kuwa unatakiwa kuwa na mpango kazi wa biashara, kuwa na bajeti na kuiheshimu bajeti yako, andaa muda wa kuiendeleza biashara yako na muda wa kuyafikia malengo utakayojiwekea.

Kubali mabadiliko

Unapokuwa na wazo na mpango kazi nadharia, inaweza kuwa ngumu kwako kukubali mahitaji yake endapo yatakuwa makubwa tofauti na unavyotegemea. Unatakiwa kuwa muwazi na kukubali mabadiliko katika safari yako nzima ya kibiashara, kwa maana kufanya hivyo kutakuwa na maana kubwa katika kuondoa tofauti kati ya mafanikio na changamoto katika safari yako.

Fuata ndoto zako            

Kuwa na malengo na ndoto katika biashara yoyote kutakusaidia kutokata tamaa katika changamoto zozote utakazopitia, kama unakiamini kitu unachokifanya basi hutotetereka kwenye changamoto yoyote utakayokutana nayo na itakusaidia katika kuchanganua kati ya malengo ya biashara yako na malengo yako binafsi kama mjasiriamali.

Penda vitu vitakavyokuhamasisha

Kabla hujaanza biashara yoyote au hata ukishaianza, kuwa mtu wa kupenda kusikia vitu chanya zaidi kuliko vyenye kukatisha tamaa. Mfano unatakiwa kuwa ni mtu wa kupenda kusoma vitabu vya ujasiriamali, kusikiliza watu waliofanikiwa, kuangalia vipindi vinavyohusu mambo hayo pamoja na kuhudhuria mikutano na makongamano ya kiujasiriamali, kwa kufanya hivyo utakuwa ni mtu mwenye mipango sahihi kwa kila kitu unachokifanya na kuyafikia malengo yako.