Wafanyakazi waongoza kwa magonjwa ya akili

Jumatano , 10th Oct , 2018

Siku ya afya ya akili duniani huadhimishwa tarehe 10,Oktoba ya kila mwaka, ambapo kauli mbiu ya Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka huu ni "Vijana na afya ya akili katika ulimwengu wa mabadiliko". Kwa mujibu wa WHO, zaidi ya watu milioni 35 duniani wanaishi na magonjwa ya akili yanayotajwa

kusababishwa na matumizi ya madawa ya kulevya, unyanyapaa na umasikini uliopitiliza.

katika kuangalia suala la ugonjwa wa akili leo tunaangazia jinsi gani wafanyakazi wanavyoathiriwa na matatizo ya afya ya akili katika mazingira yao ya kazi.

Ambapo www.eatv.tv  imemtafuta mtaalamu na mwana saikolojia wa afya ya magonjwa ya akili kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam, Bi. Neema Mwankina ambaye amesema kuwa maeneo mengi ya kazi waajiriwa hukumbwa na ugonjwa huo kutokana na mawazo pamoja na mrundikano wa kazi nyingi pasipo kupata muda wa kupumzisha akili.

"Hali kama hii inawatokea watu wengi sana maeneo ya kazini lakini wengi wao wameshindwa kujigundua kama wana tatizo la afya ya akili, utakuta kila siku bosi anakuita anakuambia hufanyi vizuri lakini utakuta wewe unajiona unafanya kazi kwa ufanisi,unaamua kujitathimini na kufanya kazi kwa bidii, lakini bado unaambiwa perfomance (utendaji wa kazi) yako ni mbovu. Hapo ndo unakumbwa na msongo wa mawazo, hali inayopelekea ugonjwa wa akili", amesema Bi Mwankina.

Aidha Bi Mwankina amesema waafrika wengi wana dhana potofu ya kuhusisha maswala ya kazi na ushirkina bila kujua hali hiyo mara nyingi huchangiwa na suala la ugonjwa wa akili.

"Maeneo mengi sana sio ya kazini peke yake hata kwenye biashara utakuta watu wanafanya kazi wanakosa wateja, hakuna wanunuzi na hawaendelei kibiashara, hasa pale akiona mtu wake wa karibu anafanikiwa kila kukicha. Sasa hali hiyo ndio inapelekea mtu kujihisi kwamba fulani ameniroga bila kujua kwamba unamatatizo", ameongeza.

Ili kutokumbwa na msongo wa mawazo unaopelekea kupata ugonjwa wa akili maeneo ya kazi, Bi Mwankina amasema ni lazima kwa wafanyakazi kujitengea muda wa kuchunguza hali zao, kujitathimini kiafya na kuwataka kulipa kipaumbele suala la afya ya akili kwani imekuwa ni tatizo kubwa linaloweza kupelekea kifo endapo halitotatuliwa mapema.