Alhamisi , 26th Sep , 2019

Watu wenye ulemavu wanaoishi maeneo ya Mzimuni, Kawe Jijini Dar es Salaam wameilalamikia serikali ya mtaa huo kuwaandikisha majina kwa ajili ya kupata msaada wa vitendea kazi na usafiri wa bajaji ili kujikwamua kibiashara lakini wanaishia kudanganywa.

Pili Adam

Wakizungumza na EATV & EA Radio Digital, wananchi hao wamesema kuwa Serikali ya mtaa imekuwa ikiwafuata na kuwaandikisha majina ili wapewe bajaji lakini mwisho wa siku wamekuwa wakiachwa kwenye vikao vya mwisho vya maamuzi ilhali wao ni wahusika wakuu.

"Serikali yetu ya mtaa inaishia kutuandikisha tu majina na kutuambia mtaletewa msaada lakini vikitokea vikao vya walemavu wanaenda wao wazima, walemavu wa Kawe wote masikini hakuna mwenye nafuu hata mmoja",  amesema Pili Adam ambaye ni moja ya watu wenye ulemavu wanaoishi mtaa huo.

Aidha, Pilli Adam ameongeza kuwa msaada mkubwa ambao utawasaidia wao ni kupatiwa bajaji, zitakazowawezesha katika usafiri na hata kujipatia kipato tofauti na kupewa pesa mkononi.

Hata hivyo EATV&EA Radio Digital imemtafuta Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mzimuni, Hassan Ngonyani ambaye amekanusha taarifa hizo na kusema.

"Mimi hiki kitu sikijui kabisa, mimi nilishawagawiaga maeneo kwa ajili ya uzalishaji mali ili waweze kujipatia rizki lakini wameuza yale maeneo", ameeleza Mwenyekiti wa mtaa huo.