Jumanne , 16th Oct , 2018

Klabu ya Simba imepata pigo lingine baada ya kigogo wake, Zacharia Hanspoppe kunaswa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Zacharia Hanspoppe

Hanspoppe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, alinaswa juzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) baada ya kuwasili nchini akitokea Dubai.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TAKUKURU, inaelezwa kuwa leo Jumanne, Hanspoppe ataunganishwa kwenye kesi inayowakabili Rais wa Simba, Evans Aveva na Makamu wake Geofrey Nyange 'Kaburu'.

Mwingine ambaye Mahakama ilitoa hati ya kukamatwa kwake ni Franklin Lauwo ambaye alipewa tenda ya ujenzi wa uwanja wa Simba uliopo Bunju jijini Dar es Salaam.

Miezi michache iliyopita Mahakama ilitoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi huyo baada ya mwendesha mashtaka wa TAKUKURU kudai kuwa wamemtafuta bila mafanikio kwa kipindi kirefu.

Aveva na Kaburu walikamatwa mwaka uliopita na kufunguliwa mashitaka ya kughushi nyaraka na utakatishaji fedha, bado wapo rumande huku kesi yao ikiendelea.