Jumatatu , 10th Dec , 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amesema hafurahishwi na vitendo vya baadhi ya askari kukamata magari ya abiria na mizigo kisha kuyachelewesha kwa muda mrefu.

Rais Magufuli kushoto, pamoja na picha ya askari wa usalama barabarani wakiwa wamesimamisha basi la abiria.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam, kwenye Kikao cha kazi kati yake na Viongozi wa TRA pamoja na wakuu wa mikoa nchini, ambapo amekemea baadhi ya vitendo vinavyoharibu biashara za watu na kukwamisha ulipaji kodi.

''Askari anaweza kujisikia tu kusimamisha gari hata kwa zaidi ya saa 6 kisha akaliachia bila kujali kuwa hao ni wafanyabiashara na wanajisikia vibaya, kuharibiwa biashara zao wakapata hasara na mwisho wa siku wasilipe kodi. Mara nyingi hili linafanywa na jeshi la polisi'', amesema Rais.

Aidha Rais Magufuli ametoa agizo kwa mamlaka mbalimbali zinazohusika na kodi kuhakikisha zinaondoa vikwazo kwa walipa kodi pamoja na wawekezaji kutoka nje ya nchi.

''Pia nawataka TPA, TRA, Jeshi la polisi, Idara ya uhamiaji mjirekebishe kuna vitendo vingi vya kukwamisha wawekezaji na walipa kodi naomba mlifanyie kazi hilo nafahamu mengi kwahiyo mbadilike'', ameongeza.