Alhamisi , 11th Oct , 2018

Suala la matokeo limekuwa ndiyo gumzo kubwa hivi sasa kwa klabu ya Manchester United, ambapo mpaka sasa imeshinda michezo minne pekee katika ligi msimu huu, ikipoteza michezo mitatu na sare moja.

Si msimu huu pekee, hata katika misimu kadhaa ya nyuma tangu aondoke Sir Alex Ferguson, klabu hiyo imekuwa haifanyi vizuri katika michuano yote inayoshiriki ukiondoa msimu uliopita ambapo ilimaliza nafasi ya pili katika ligi. Lakini swali ambalo unaweza kujiuliza, ni kwanini inaendelea kulipa mishahara na kusajili wachezaji wa bei kali duniani?.

Fahamu hapa kuwa Manchester United ndiyo klabu pekee yenye wadhamini wengi kuliko klabu zote barani Ulaya, ina jumla ya wadhamini 68 ambao huchangia faida ya takribani Pauni 269 millioni kwa mwaka kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2018 iliyotolewa na kampuni ya masuala ya michezo na burudani ya CSM.

Hiyo ndiyo sababu klabu hiyo inaendelea kuwa na nguvu zaidi nje ya uwanja licha ya changamoto zote inazozipitia katika miaka hii ya karibuni. Klabu zingine zinazofuatia kwa mujibu wa ripoti hiyo ni pamoja na, Barcelona inayoingiza Pauni 261 millioni kwa idadi ya wadhamini 43, Bayern Munich yenye wadhamini 29 ambayo inavuna jumla ya Pauni 180 millioni na Real Madrid katika nafasi ya nne, ikiwa na wadhamini 19 ambao wanaipa jumla ya Pauni 178 millioni kwa mwaka.

Nafasi ya tano ikishikiliwa na Chelsea yenye wadhamini 18 ambao huiingizia klabu hiyo jumla ya Pauni 154 millioni, nafasi ya sita ni Manchester City, ya saba ni Arsenal huku nafasi ya nane, tisa na ya kumi zikishikiliwa na Liverpool, PSG na Juventus.