Jumatatu , 11th Feb , 2019

Nahodha msaidizi wa klabu ya Simba, Mohamed Hussein 'Tsahabalala' amesema alichokigundua katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika ni kuwa kila klabu inashinda michezo yake ya nyumbani.

Mohamed Hussein

Mohamed Hussein ameyasema hayo katika mkutano na wanahabari kuelekea mchezo dhidi ya mabingwa mara 8 wa michuano hiyo, Al Ahly ambao utapigwa kesho (leo) Jumanne katika uwanja wa taifa Jijini Dar es salaam.

"Kesho (leo) tuna mechi muhimu, sisi tumejipanga vizuri ukizingatia mechi ya kwanza tulipoteza na tulipoteza kwa goli nyingi. Sasa hivi na sisi tupo nyumbani, kama wao walivyokua nyumbani tumejipanga kupata points 3", amesema Mohamed Hussein. 

"Tulichokiona timu nyingi zinashinda kwenye uwanja wa wake wa nyumbani, hilo ndio jambo ambalo sisi wachezaji wa Simba linatupa moyo zaidi", ameongeza.

Simba ipo nafasi ya tatu katika kundi 'D' kwa pointi tatu huku Al Ahly ikiongoza kundi kwa pointi 7. Nafasi ya pili inashikiliwa na AS Vita Club kwa pointi zake nne na JS Saoura ikiburuza mkia.