Ally afunguka tetesi za Simba na Yanga

Jumanne , 13th Mar , 2018

Baada ya kuonesha kiwango kizuri siku za hivi karibuni hali iliyopelekea kuwepo kwa tetesi za kutakiwa na timu kubwa nchini za Simba na Yanga, mlinzi wa klabu ya Stand United Ally Ally, amesema yeye bado ana mkataba na timu yake.

“Siwezi kuzungumzia kama nipo tayari kuungana na moja ya timu hizo, bado nina mkataba na Stand United, kama wananihitaji wafuate taratibu zilizopo'', alisema Ally baada ya mchezo wa jana dhidi ya Yanga ambapo timu yake ilipoteza 3-1.

Ally Ally alionesha kiwango kizuri katika mechi mbili alizocheza kwenye uwanja wa taifa dhidi ya vinara wa ligi Simba, ambapo timu hizo zilitoka sare ya 3-3 huku pia akisimama imara kwenye mchezo wa jana dhidi ya Yanga licha ya kujifunga bao lakini aliweza kurejea mchezoni na kucheza vizuri.

Kwa upande wake kocha msaidizi wa Stand Unioted amesema Ally ni mchezaji mzuri na ana nidhamu ya hali ya juu hivyo milango ipo wazi kwa timu kumsajili lakini ni lazima wafuate taratibu zote.

''Uongozi haUwezi kumzuia kwani kinachohitajika ni makubaliano ya pande zote mbili, mana akiondoka atataoa nafasi kwa vijana wengine kupata nafasi ya kucheza na kuonesha kiwango kama yeye'', amesema.