Jumatatu , 15th Oct , 2018

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Emmanuel Amunike amebadili mfumo wa uchezaji wa timu hiyo kuelekea mchezo wa marudiano kuwania kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika AFCON dhidi ya Cape Verde kwa kujikita zaidi kwenye mbinu za kushambulia.

Kikosi cha Taifa Stars kushoto na kocha Emmanuel Amunike kulia.

Mipango hiyo ya kocha Amunike ambaye atakuwa anaiongoza Stars kwa mara ya kwanza katika mchezo wa nyumbani, imewekwa wazi na meneja wa kikosi hicho, Danny Msangi ambaye amesema maelekezo ya mwalimu huyo kwasasa yanalenga kushambulia zaidi.

"Huu ni mchezo wa kwanza wa nyumbani kwa kocha Amunike, amejikita kwenye kushambulia zaidi tofauti na michezo miwili tuliyocheza ugenini, hapa tunatafuta ushindi tena wa mabao mengi kwahiyo kila kitu kimebadilika mkazo upo kwenye kushambulia", amesema.

Aidha Msangi ameongeza kuwa mbinu nyingine ambayo mwalimu anaifanyia kazi ni kuhakikisha timu hairuhusu bao hata moja dhidi ya wapinzani wake ili kujiweka kwenye mazingira ya kusonga mbele.

Taifa Stars ambayo ipo Kundi L na timu za Uganda, Cape Varde na Lesotho, imeshacheza michezo mitatu na kutoa sare mbili dhidi ya Lesotho nyumbani na Uganda ugenini kabla ya kupoteza 3-0 dhidi ya Cape Verde.

Amunike amemuongeza kikosini, mlinzi mkongwe wa Simba SC, Erasto Edward Nyoni, ambaye ana uwezo wa kucheza kama kiungo pia. Taifa Stars itashuka dimbani kesho kucheza na Cape Verde kwenye mchezo wake wa 4 kundi L.