Jumanne , 17th Jul , 2018

Klabu ya Arsenal imejikuta katika janga la kusainishwa mkataba feki na kampuni ya magari ya umeme ya nchini China ya BYD na afisa aliyejifanya kuwa ni mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Wachezaji wa Arsenal wakitambulisha jezi yenye jina la kampuni hiyo

Arsenal ilisaini mkataba na kampuni hiyo mwezi Aprili, 2018, ambapo miezi mitatu baadaye imegundulika kuwa afisa ambaye klabu ilisaini mkataba naye hakuwa mfanyakazi ndani ya kampuni hiyo.

Mshukiwa huyo aliyejulikana kwa jina la, Li Juan yuko katika kizuizi kwa sasa kutokana na uchunguzi ambao unaoendeshwa na maafisa wa Polisi .

Ripoti zinasema kwamba mshukiwa huyo alikopa bidhaa za kampuni katika mji wa Shanghai  nchini China kwaajili ya kushawishi washirika mbalimbali ili kuingia nao mikataba kwa kutumia jina la kampuni ya BYD.

Picha ya pamoja ya klabu ya Arsenal na kampuni ya BYD

Katika mkataba huo, klabu ya Arsenal na Li Juan kupitia kwa BYD walikubaliana kuitangaza kampuni hiyo katika mbao za matangazo za klabu ndani ya uwanja wa Emirates pamoja na siti za kukalia katika uwanja huo.

BYD ni kampuni ya kichina inayosimamia kubuni, kuendeleza, kutengeneza na kusambaza magari ya umeme, mabasi na magari ya makubwa ya kibiashara ambayo ina wafanyakazi zaidi ya 220,000 dunia nzima.

Sintofahamu ilianza baada ya kampuni hiyo kutoa taarifa, Julai 12 inayokana kuhusika kwake katika biashara yoyote na Li Juan au kampuni nyingine ambayo imepelekea pia kushuka kwa hisa za kampuni hiyo kwa asilimia 5.7.