Jumapili , 21st Jun , 2020

Klabu ya Azam FC imejinasibu kuibuka na ushindi dhidi ya Yanga pamoja na kutaja udhaifu wa wapinzani wao kuelekea mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa leo katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Azam FC na Yanga

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha klabu hiyo, Thabit Zakaria 'Zakazakazi' ambapo amesema kuwa klabu hiyo imejipanga kuibuka na ushindi leo kwa sababu Yanga ina kikosi cha kawaida.

"Yanga imezifunga timu zingine mara nyingi zaidi kuliko ilivyoifunga Azam FC, tumewafunga mara 8 na wao wametufunga mara 8 kati ya mara 23 tulizokutana nazo katika ligi, hivyo leo tutawafunga kwa mara ya tisa na kuwaacha na idadi yao", amesema Zakazakazi.

"Yanga haina kikosi cha ushindani ndio maana inatoa sana morali ya pesa kwa wachezaji wao ili wapate ushindi, ninawaambia kuwa hizo pesa bora wakatoe hata misaada maana hawatapata ushindi", ameongeza.

Azam FC inakamata nafasi ya pili ikiwa na pointi 57 katika michezo 29 huku Yanga ikikamata nafasi ya tatu ikiwa na pointi 55 baada ya michezo hiyo 29.