Jumatano , 1st Apr , 2020

Uongozi wa klabu ya Azam FC umeeleza kukoshwa na kazi ya mshambuliaji wa sasa wa Simba, John Bocco huku ikimfungulia milango kurejea wakati wowote ndani ya klabu hiyo.

Mshambuliaji wa Simba, John Bocco

Bocco ambaye ni nahodha wa Simba, alijiunga msimu wa 2017/18 akitokea Azam FC ambako aliitumikia kwa takribani miaka tisa, tangu mwaka 2008 ambao klabu hiyo ilipanda daraja kwa mara ya kwanza.

Akizungumzia kuhusu kiwango cha mshambuliaji huyo, Ofisa Habari wa Azam FC, Zaka Zakazi amesema kuwa ni mchezaji mzuri na kwamba ni wakati sahihi wa nyota huyo kurejea Azam kuendelea na soka lake.

"Bocco ni mchezaji mzuri na ana uwezo mkubwa akiwa uwanjani kwani anachokifanya kinaonekana, kwa sasa ni wakati wake akihitaji kurejea Azam FC ili kurejea nyumbani," amesema Zaka Zakazi.

John Bocco ni mchezaji Mtanzania aliyefunga mabao mengi ya ligi kuu kuliko wote wanaocheza hivi sasa, akiwa amefunga mabao takribani 120. Msimu huu ndani ya Simba, Bocco amefunga mabao manne na kutoa pasi mbili za mabao.