Jumanne , 16th Oct , 2018

Msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara ametoa ujumbe wake wa kwanza tangu aachiwe huru na polisi baada ya kuwa chini ya ulinzi kwa muda akihojiwa kuhusu kutekwa kwa mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji 'Mo'.

Haji Manara kushoto na Mohammed Dewji kulia.

Manara ambaye alikuwa miongoni mwa watu 26 wanaoshikiliwa na jeshi la polisi kwaajili ya mahojiano, ameachiwa leo Oktoba 16, 2018. Baada ya kuachiwa Manara amesema watu waendelee kumuombea Mo Dewji aweze kupatikana.

''Kila jambo huja na sababu yake, na mitihani ya kilimwengu tumeumbiwa sisi binaadamu, naendelea kuwasihi tuviache vyombo vinavyohusika vitimize wajibu wao, kubwa tuendeleze dua na sala kwaajili ya kiongozi wetu InshaAllah'', ameandika Manara.

Mwishoni wa wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alilitaka Jeshi la Polisi kuharakisha upelelezi wake ili lisiwashikilie washukiwa kwa zaidi ya saa 24.

Mohammed Dewji ambaye ni mwanahisa mkuu wa klabu ya Simba akimiliki asilimia 49 ya hisa, alitekwa alfajiri ya Oktoba 11, 2018 maeneo ya Masaki jijini Dar es salaam.