Jumapili , 17th Mar , 2019

Simba imeweka historia nyingine kwa Tanzania baada ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika jana katika Uwanja wa Taifa.

Kushoto, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohamed Dewji akishangilia ushindi wa Simba.

Kwenye mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya AS Vita, Simba ilihitaji ushindi wowote ili ifuzu hatua ya robo fainali, jambo ambalo lilifanikiwa kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, mabao yaliyofungwa na Mohamed Hussein katika dakika ya 36 na Clatous Chama katika dakika ya 90 huku bao pekee la AS Vita likifungwa na Kasendu Kazidi katika dakika ya 13.

Kabla ya mchezo huo, Afisa Habari wa Simba, Haji Manara aliahidi kupitia kipindi cha Kipenga Xtra cha East Africa Radio kuwa endapo klabu yake itaibuka na ushindi, hatowasema mahasimu wake Yanga kama alivyokuwa akifanya hapo awali, bali atakaa kimya.

"Mashabiki wa Yanga wananihofia sana mimi, wanaogopa kuisapoti Simba kisa eti mimi nitasemaje. Sasa naahidi Simba ikishinda sitowasema Yanga, nitaishia kusema tu 'Alhamdulillah'", alisema Manara, Ijumaa, Machi 15.

Lakini kinachoonekana hivi sasa baada ya ushindi huo ni muendelezo wa maneno yake ya utani kwa mahasimu wake ambao amesema walikuwa wakiidharau timu yake.

Ahadi nyingine ambayo aliihidi Manara ni kuwa endapo mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara watavuka hatua hii ya makundi na kwenda robo fainali, basi yatakapomalizika mashindano hayo mwezi June, yeye ataitwa Msemaji wa Mabingwa wa Afrika.

Simba imevunja rekodi yake yenyewe kuwa klabu ya kwanza Tanzania tangu mwaka 1974 kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika, ambapo sasa itaungana na timu za Waydad Casablanca, Mamelodi Sundowns, TP Mazembe, SC Constantine, Horoya, Esperance Tunis pamoja na Al Ahly.

Bonyeza hapa chini kutazama zaidi.