Jumatano , 19th Sep , 2018

Kocha mkuu wa Stand United, Amars Niyongabo amesema kuwa tuhuma anazozopelekewa kuwa anapendelea wachezaji wa kigeni kuliko wazawa aliowakuta kikosini sio za kweli kwakuwa anazingatia juhudi za mchezaji.

Kikosi cha Stand United.

Niyongabo ambaye aliwahi kuifundisha timu ya taifa ya Burundi ( Intamba Murugama) na Kenya (Harambee Stars) alijiunga na Stand United mwanzoni mwa msimu uliopita na kuisaidia klabu hiyo kutokushuka daraja, ikimaliza nafasi ya 11 ya msimamo wa ligi kwa alama 32.

Akizungumza na www.eatv.tv  kuhusu tuhuma hizo za kupendelea wachezaji wa kigeni zaidi kuliko wazawa, Niyongabo amesema,

Kwanza mimi huwaga sina mambo ya hivyo, huwa nawatumia sana wachezaji ninaowakuta katika klabu ili nao wapandishe vipaji vyao lakini nimekuta baadhi ya wachezaji wa Kitanzania hawajielewi, hawajui wanatakiwa kufanya nini katika soka kwakuwa wanaridhika mapema”.

Sasa wakipata ushindani, itaamsha ile hari yao ya kujua kwamba wanatakiwa kufanya vizuri kwahiyo ninafanya hivyo ili waamke  kwa maana kwamba kama tuko Tanzania basi na soka lake linatakiwa lipande ”, ameongeza Niyongabo.

Kuhusu uwezo wa mchezaji aliyefunga ‘Hat-Trick’ ya kwanza msimu huu kwenye mchezo dhidi ya Yanga, Alex Kitenge, kocha huyo amesema kuwa amempa nafasi mchezaji huyo katika kikosi chake kwakuwa anamfahamu na amemfundisha tangu akiwa mdogo nchini Burundi na anamtabiria kuwa atafanya makubwa katika ligi kuu.

Pia kocha huyo amesisitiza kuwa ataendelea kuwaamini vijana ambao wana vipaji bila kujali nchi wanazotokea, akiwatolea mfano vijana ambao amewapa nafasi  kama,Tarik Seif aliyemtoa ligi daraja na kwanza na Ally Ally ambaye ametokea ligi daraja la pili Zanzibar.

Stand United itakuwa ugenini kupambana na KMC, Ijumaa ya wiki hii katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara. Mpaka sasa inakamata nafasi ya tisa ya msimamo, ikiwa na alama sita katika michezo yake minne iliyocheza, ikishinda mechi mbili na kupoteza mechi mbili.