Ijumaa , 18th Oct , 2019

Baada ya Shirikisho la soka Hispania (RFEF), kuvitaka vilabu vya Barcelona na Real Madrid vipendekeze tarehe mpya ya ElClasco, Barcelona ambao ndio wanatakiwa kuwa wenyeji wa mchezo huo wamependekeza uchezwe Desemba 18, 2019 Camp Nou.

Uwanja wa Camp Nou

Taarifa iliyotolewa na Barcelona muda mfupi baada ya maamuzi ya Bodi ya La Liga (LFP) kuhusu mabadiliko ya kusogeza mbele mchezo huo kutoka Oktoba 26, kama ilivyokuwa imepangwa awali.

'Sisi hatukutaka mchezo huo upelekwa Santiago Bernabeu kama ambavyo LFP na RFEF walipendekeza, hivyo umerudishwa Camp Nou na tunapendekeza Desemba 18, 2019', imeeleza taarifa ya Barcelona.

Katika upande mwingine Barcelona wameweka wazi kuwa wao walikuwa na imani na mashabiki wao hata kama mchezo ungebaki Oktoba 26, ungechezwa kwa amani na hawana tabia ya fujo zaidi tu ya kufurahia.

Pia wameeleza kuwa kwasasa wanafanya taratibu za mwisho kuhakikisha wanaanza kurejeshga fedha za mashabiki ambao tayari walikuwa wameshakata tiketi kuhudhuria mchezo huo wa La Liga.

Hivi karibuni viongozi 9 wa siasa wa Catalunya wamehukumiwa jela miaka 9 mpaka 13 kwa kukutwa na hatia ya uchochezi waliofanya mwaka 2017 katika azimio la kudai uhuru wa jimbo la Catalunya.

Baada ya hukumu hiyo, wananchi wa jimbo hilo wamekuwa wakifanya maandamano kupinga hukumu hizo.

Maandamano mengine yamepangwa kufanyika siku hiyo ya Oktoba 26, na hivyo kupelekea shirikisho la soka la Hispania (RFEF) leo kutangaza kuahirisha mechi hiyo ya El Clasico.