Jumanne , 19th Mei , 2020

Beki kisiki wa Coastal Union, Bakari Ndondo Mwamnyeto amezungumzia kuhusu kutaka kusajiliwa na klabu ya Yanga kuelekea dirisha kubwa la usajili la msimu ujao.

Hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa tetesi nyingi katika siku za karibuni, akitajwa kutaka kusajiliwa na mabingwa hao wa kihistoria nchini kutokana na kiwango kikubwa alichokionesha msimu huu.

Awali, beki huyo alikuwa anawaniwa vikali na Simba iliyokuwa na mipango ya kumsajili katika kuiboresha safu yao ya ulinzi inayoongozwa na Pascal Serge Wawa na Erasto Nyoni kabla ya kushindwana kwenye dau la usajili ambalo ni Sh Mil. 100 ambayo klabu ya Coastala Union inahitaji.

Akizungumzia kuhusu taarifa hiyo, Mwamnyeto amesema,“ni mapema kuzungumzia wapi ninakwenda, kwani bado muda wa usajili na isitoshe bado nina mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea Coastal Union".

Nipo kwenye mazungumzo mazuri na Yanga, kikubwa ninachokiangalia hivi sasa ni maslahi pekee yatakayonifanya nisaini Yanga, nafahamu zipo klabu nyingine zilizokuwa kwenye mipango ya kuwania saini yangu lakini nimeshindwana nazo katika maslahi na siyo kingine,” amesema Mwamnyeto.

Kwa upande wa Yanga, leo Mei 19, 2020 inatarajia kuzindua kampeni ya mabadiliko makubwa ya klabu hiyo, ambayo itahusisha uwekezaji pamoja na kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu kama ambavyo mahasimu wao Simba wanaendelea nao.