Alhamisi , 2nd Apr , 2020

Bodi ya Wakurugenzi wa Ligi Kuu nchini Ubelgiji 'Jupiter Pro League' imekubaliana kwa pamoja kumaliza msimu wa ligi 2019/20 na kuipatia ubingwa Club Brugge iliyokuwa inaongoza ligi hiyo.

Klabu ya soka ya Club Brugge

Hatua hiyo imefikiwa kufuatia kuendelea kusambaa kwa virusi hatari vya Corona barani Ulaya na kupelekea kusimamishwa kwa mashindano mbalimbali barani humo.

Ligi ya Ubelgiji imekuwa ligi ya kwanza kufikia maamuzi hayo huku nchi nyingi zikisubiri hali endapo itakuwa shwari hapo baadaye ili ziweze kumalizia msimu. Kwa  mujibu wa wakurugenzi waliopiga kura kuamua msimu wa ligi nchini humo, wamesema kuwa suala la haki za matangazo ya ligi hiyo litajadiliwa April 15.

Ligi Kuu ya Soka nchini Hispania LA Liga ilipitisha uamuzi wiki iliyopita kuwa mechi zilizobakia hazitachezwa hadi hapo virusi vya Corona vitakapomalizika, hali ikiwa hivyo hivyo kwa nchi ya Italia ambayo ndiyo yenye maambukizi mengi ya virusi vya Corona barani humo, huku idadi ya vifo ikiwa ni zaidi ya 13000.

Chama cha soka nchini Uingereza FA kinatarajia kukaa pamoja na klabu zote za ligi hivi karibuni kujadili juu ya mustakabali wa ligi kuu nchini humo EPL na ligi daraja la kwanza 'Championship'.