Jumapili , 10th Nov , 2019

Bondia Dwight Ritchie raia wa Australia amefariki, huko jijini Melbourne, muda mfupi baada ya kumaliza mazoezi yake ya kawaida.

Dwight Ritchie

Promota aliyekuwa akisimamia mapambano ya Ritchie, Jake Ellis, amethibitisha kifo cha bondia huyo ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 27.

"Ni huzuni kubwa na mshtuko mkubwa kutangaza kifo cha mpambanaji Dwight Ritchie, ambaye amefariki akiwa anafanya kitu anachokipenda'', Jake Ellis  ameiambia BBC Sport.

Ritchie alikuwa ameshacheza mapambano 21, ambapo kati ya hayo alipoteza mawili tu, moja ikiwa ni lile la hivi karibuni dhidi ya Tim Tszyu kuwania taji la IBF Australia kwenye uzito wa 'Super-welterweight' mapema mwezi Agosti.

Katika mazoezi hayo Ritchie alikuwa anafanya na bondia Michael Zerafa, ambaye anajiandaa kwa pambano la marudiano na Jeff Horn, ambaye ni bingwa wa zamani wa WBO Welterweight.