Chama amuomba msamaha Feisal Toto

Jumanne , 10th Mar , 2020

Mchezaji wa klabu ya Simba Clatous Chama,  amemuomba msamaha mchezaji wa klabu ya Yanga Feisal Salum maarufu Fei Toto, kufuatia kitendo cha kumkanyaga kwa makusudi mguuni wakati  wa pambano lao likiendelea siku ya Machi 8,2020.

Kushoto mchezaji wa Simba Chama, kulia Fei Toto wa Yanga

Chama amemtaka radhi Fei Toto kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, ambapo ameeleza tayari ameshaongea na Feisal kumuomba msamaha na amekubaliwa ombi lake kwa sababu mpira ni burudani sio uadui.

"Wapendwa mashabiki wa mpira wa miguu, napenda kuwashukuru wote kwa mchezo wa dabi yetu, naumia tumepoteza mchezo lakini kilichotokea kati yangu na Feisal ilikuwa ni kutafuta matokeo uwanjani, nimeshaongea naye na amenikubalia ombi la msamaha, naahidi kuwa balozi mzuri wa mchezo ndani ya uwanja, ahsanteni sana"  ameandika Clatous Chama.  

Mchezo huo wa watani wa jadi ulimalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Simba, kwa goli ambalo lilifungwa na Benard Morisson katika dakika ya 44 kipindi cha kwanza.