Ijumaa , 17th Sep , 2021

Kocha wa 'Wekundu wa Msimbazi' Simba, Mfaransa Didier Gomez Da Rosa amefunguka na kusema kuwa, ameridhika kwasababu walichokuwa wanakitaka kwenye maandalizi ya michuano yote ya msimu ujao tayari wameshakipata.

Kocha wa Simba, Didier Gomez Da Rosa akiwa mazoezini.

Gomez ameyasema hayo wakati Simba walipomaliza mazoezi yao ya mwisho Septemba 16, 2021 kabla ya kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam Ijumaa ya leo Septemba 17, 2021 kwa ajili ya tamasha la Simba Day linalotaraji kufanyika Jumapili ya Septemba 19, 2021 kwenye dimba la Mkapa.

Gomez amesema; "Michezo miwili ya kirafiki tuliyocheza huku imetuonesha wapi tulipo kwa sasa, tunarejea DSM kwa ajilibya mchezo wetu na TP Mazembe pamoja na maandalizi ya mwisho mwisho kuelekea kwenye Ligi kuu, nashukuru tulichokuwa tunakitaka kwenye kambi tumefanikiwa kukipata".

Simba ilianza maandalizi ya msimu ujao Agosti 10 mwaka huu waliposafiri na kwenda kuweka kambi ya wiki mbili nchini Morocco na kucheza michezo miwili ya Kirafiki dhidi ya FAR AS Rabaat ya Ligi kuu nchini humo na timu ya daraja la kwanza, Olympique na kupata matokeo yote ya sare.

Baada ya hapo, msafara ulirejea nchini mwishoni mwa mwezi Agosti na kutimkia jijini Arusha ambapo ilicheza michezo mitatu ya kirafiki, dhidi ya Coastal Union na kuto sare ya bila kufungana na kupata ushindi mbele ya Fountain Gate na Mabingwa Burundi, Aigle Noir.