Jumanne , 18th Jun , 2019

Katika wakati ambao Afisa Habari wa klabu ya Yanga, Dismas Ten amekuwa na furaha kupita nyakati zote ni huu.

Dismas Ten na Haji Manara

Yawezekana ni kutokana na mchakato wa uchangiaji wa klabu hiyo kuonekana kufanikiwa kwa asilimia zaidi ya 99, hasa katika hafla ya mwisho iliyofanyika wikiendi iliyopita maarufu kama 'Kubwa Kuliko', ambayo ilikusanya zaidi ya Sh. 800 milioni.

Tunaweza kusema kwamba hivi sasa Yanga inakwenda katika 'right direction' kama ulivyo msemo maarufu wa Rais Dkt. John Magufuli katika mikutano yake mbalimbali. Mpaka sasa Yanga inaelekea kumaliza idadi ya wachezaji wa kigeni wanaoruhusiwa kusajili kwa mujibu wa sheria za Bodi ya Ligi, imeshawasajili Patrick Sibomana, Lamine Moro, Issa Bigirimana, Maybin Kalego, Mustapha Suleiman, Juma Balinya, Sadney Urikhob na Abdulaziz Makame.

Mara baada ya kumalizika kwa hafla ya 'Kubwa Kuliko' wiki iliyopita, Dismas Ten amepandisha posti takribani 10 ambazo zinaonesha jinsi gani ambavyo amejipanga upya kujibu mashambulizi ya mpinzani wake, Afisa Habari wa Simba, Haji Manara.

Kutokana na kasi hiyo, licha ya timu zote kubwa Simba na Yanga kuonesha dalili zote za ushindani ndani ya uwanja msimu ujao kutokana na usajili wanaoufanya, pia utashuhudiwa ushindani nje ya uwanja kwa wasemaji hawa wa vilabu vikubwa zaidi Tanzania.

Pia kwa dalili hizo, msimu ujao timu hizo kubwa zitakuwa vizuri kiuchumi, hali ambayo inampa ujasiri Dismas kiasi cha kuanza kujibu mashambulizi ya mashabiki wa Simba.