Alhamisi , 6th Feb , 2020

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa siku tatu kwa Baraza la Michezo nchini BMT kufuatilia kwa ukaribu malalamiko yote ya wadau wa soka katika ligi kuu na ligi zingine.

Waziri Dkt. Harrison Mwakyembe

Waziri Mwakyembe amefikia hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa soka kutokana na kile kinachoendelea katika Ligi Kuu Tanzania bara na Ligi Daraja la Kwanza bila ya majibu yoyote kutoka kwa wahusika.

Akizungumza baada ya kutoa agizo hilo, Waziri Mwakyembe amesema, "tumepata malalamiko siyo ya waamuzi pekee, ila hata kwa mambo mengine mfano timu inasahaulika kwenye ratiba na mambo mengine na wahusika hawachukui hatua, serikali haiingilii soka lakini yakizidi lazima tuingie tutoe muafaka".

"Tukiamua tucheze soka tucheze soka, serikali ya awamu ya 5 siyo ya ubabaishaji, wadau wanaisumbua Wizara kutuletea barua kila siku. Nimeiagiza BMT wakae wajue kuna nini huko, wakishindwa kupata muafaka. Mimi mwenyewe nitaingilia kati".

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara pia amezungumzia kuhusiana na mwenendo wa waamuzi nchini, amesema kuwa matukio hayo hayapo kwa Simba pekee kama baadhi ya watu wanavyodai.

"Haya maamuzi hayafanyiki kwenye mechi ya Simba tu, jambo la jana lingetokea kwa Simba watu wangesema Simba wanabebwa... lakini kwakuwa imetokea kwa Yanga wanasema ni makosa ya mwamuzi. Lazima mjue kuwa waamuzi ni binadamu, inawezekana uwezo wao ni mdogo au ni makosa tu", amesema Manara.