Jumanne , 22nd Mei , 2018

Baada ya sintofahamu kwa wiki kadhaa hatimaye klabu ya soka ya Singida United imethibitisha kuachana na kocha wake mkuu Hans van der Pluijm, mwisho wa msimu huu baada ya kufikia makubaliano maalum baina ya pande zote mbili.

Akiongea na East Africa Television, Mkurugenzi wa Singida United Festo Sanga, amesema kuwa kocha huyo ameomba kuondoka baada ya kupokea ofa kubwa kutoka klabu mbalimbali za nyumbani, Africa na nje ya Africa.

''Ni kweli kocha Hans anaondoka mwishoni mwa msimu, tunasubiri fainali ya FA na baada ya hapo atatuaga rasmi. Kimsingi yeye mwenyewe ameomba kuondoka baada ya kupokea ofa kutoka kwa klabu kubwa za hapa na nje ya Africa pia'', amesema.

Kocha huyo wa zamani wa Yanga, ameiongoza Singida United msimu huu katika mechi 29 hadi sasa za ligi kuu, akishinda mechi 11, sare 11 na kufungwa mara 7. Ameisaidia timu hiyo iliyopanda ligi kuu msimu huu kushika nafasi ya 5.

Wakati huo pia amefanikiwa kuifikisha Singida United kwenye fainali ya Kombe la shirikisho nchini (ASFC), kutofungwa kwenye mechi zote 5 aa michuano hiyo hadi nusu fainali. Itacheza na Mtibwa Sugar kwenye fainali Juni 2.

Zaidi msikilize Festo Sanga hapo chini.