Jumanne , 11th Dec , 2018

Michezo ya mwisho ya hatua ya makundi ya klabu bingwa Ulaya inatarajiwa kupigwa leo na kesho, mbayo itatoa listi kamili ya timu zilizofuzu hatua ya mtoano ya michuano hiyo na zile zinazoteremka hadi katika Europa League.

Mohamed Salah (kushoto), Neymar (katikati), Dries Mertens (kulia)

Mpaka sasa jumla ya timu 12 zikiwemo Real Madrid, Manchester United, Borussia Dortmund, Bayern Munich, Atletico Madrid, Barcelona, Juventus, Manchester City na FC Porto zimeshafuzu hatua ya mtoano, zikisubiri kukamilisha tu idadi ya michezo hii leo. 

Lakini hali iko tofauti kwa baadhi ya makundi ambapo timu kadhaa hazijui hatma yake hadi hapo dakika 90 zitakapokamilika usiku wa leo.

Kundi C lenye timu za PSG, Napoli, Liverpool na FK Crvena Zvezda ndilo linalozungumziwa zaidi kutokana ushindani uliokuwepo ambapo hakuna timu yeyote yenye uhakika wa asilimia 100 ya kufuzu hatua ya mtoano mpaka sasa. Zote zinasubiri hatma ya michezo yao ya leo ili kutoa timu mbili zitakazofuzu hatua hiyo.

Napoli ina alama 9 na uwiano wa magoli ya kufunga na kufungwa ukiwa ni magoli 3. Ili iweze kufuzu hatua ya mtoano inahitaji kushinda dhidi ya Liverpool leo kwa idadi yoyote ya magoli, sare au ifungwe kwa bao moja na wakati huohuo PSG ipoteze mchezo wake.

Kwa upande wa PSG yenyewe inatakiwa kushinda dhidi ya  FK Crvena Zvezda leo, ipate sare na wakati huohuo Napoli isishinde kwa idadi ya mabao matatu au zaidi au ipate sare na wakati huohuo Liverpool isipate ushindi, ndipo inaweza kufuzu hatua inayofuata.

Liverpool ndiyo yenye wakati mgumu zaidi kuliko PSG na Napoli, ambapo inatakiwa kushinda kwa bao 1-0 au kwa tofauti ya mabao 2 dhidi ya Napoli huku ikitakiwa kutopoteza wala kupata sare kwenye mchezo huo ili iweze kusonga mbele.