Ijumaa , 10th Sep , 2021

Mchezo wa watani wa jadi kati Simba SC dhidi ya Yanga, mkondo wa kwanza unatarajiwa kucheza November 11 katika dimba la Benjamin Mkapa majira ya saa kumi na moja jioni.

Yanga na Simba walipokutana msimu uliopita

Taarifa hiyo imetolewa na mkurugenzi wa Bodi ya Ligi Kuu Nchini Tanzania, Almas Kasongo siku ya leo alipokuwa akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari za Michezo ndani ya makao makuu ya Shirikisho la soka Nchini Tanzania (TFF) juu ya ratiba ya msimu wa 2021/2022.

Kasongo amesema kuwa kuelekea msimu mpya mechi za ligi zitagawanyika katika majira tofauti ambapo ameyagwa katika makundi sita tofauti, Saa nane mchana, saa kumi kamili, saa kumi na moja jioni, saa moja usiku, saa mbili kamili usiku pamoja na mechi kadhaa ambazo bado hazijapangiwa muda maalum wa kucheza.

Vile vile baadhi ya viwanja vinaendelea kufanyiwa ukarabati ili kuweka taa zitakowezesha kuchezwa mechi muda wa usiku, ambapo viwanja ambavyo vimeainishwa ni Jamhuri Dodoma, Dimba la Kassim Majaliwa Ruangwa,CCM Mkwakwani Tanga,Kaitaba Kagera na Jamhuri Mkoani Morogoro.

Ligi hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 27 mwaka huu na kuamlizika Juni 19 mwaka 2022 huku michezo ya  ufunguzi mnamo Seeptemba 27 itashuhudiwa Mtibwa Sugar ikikabiliana na Mbeya Kwanza Fc, Namungo itamenyana na Geita Gold,Coastal Union itachuana dhidi ya Azam.