Jina linaloongoza kutajwa nafasi ya Pochettino

Jumatano , 20th Nov , 2019

Baada ya jana Novemba 19, 2019 usiku klabu ya Tottenhama kutangaza kuachana na kocha wake mkuu Mauricio Pochettino, tetesi zinazoendelea sasa ni juu ya nani atachukua mikoba ya kocha huyo raia wa Argentina.

Mauricio Pochettino

Kupitia taarifa yake Tottenham ilieleza kuwa pande mbili zimefikia makubaliano ya kuvunja mkataba wake pamoja na wasaidizi wake ambao ni Jesus Perez, Miguel D’Agostino na Antoni Jimenez.

Kuanzia usiku huo, kocha anayetajwa sana kuwania kiti hicho ni Jose Mourinho, ambaye hana timu tangu alipotimuliwa Manchester United msimu uliopita.

Mourinho amekuwa akitajwa kuwaniwa na timu mbalimbali ikiwemo za taifa lakini mara nyingi imekuwa ikielezwa kuwa yeye binafsi anazikataa ofa hizo.

Jose Mourinho

Kwa upande wake Mauricio Pochettino amekuwa akitajwa kuhitajika katika vilabu vya Real Madrid na Manchester United huku Bayern nayo ikiongezeka kwenye orodha siku za hivi karibuni baada ya kumfukuza kocha wake Niko Kovac.

Pochetino alijiunga na Tottenham, 2014 kutoka Southampton. Ameiongoza katika michezo 293. Ameshinda 159, sare 62 na kapoteza 72. Ameiacha Tottenham ikiwa nafasi ya 14 kwenye EPL na alama 14, michezo 12. Michezo 7 ya mwisho katika michuano yote Spurs wameshinda mechi mbili tu.