Jumatano , 13th Jun , 2018

Uongozi wa bingwa wa ngumi duniani uzani wa juu anayeshikilia mkanda wa WBC, Mmarekani Deontay Wilder, hatimaye amekubali kukaa meza moja na uongozi wa bingwa wa dunia anayeshikilia mikanda ya WBA, IBF na WBO Muingereza Antony Joshua tayari kwa kusaini pambano lao.

Wilder amethibitisha kukubali pambano hilo lipigwe nchini Uingereza na sio Marekani kama ambavyo alitaka awali kabla ya uongozi wa Joshua kukataa na kutaka lipigwe Uingereza. ''Ofa ya dola milioni 50 kwaajili ya mimi kupigana na Joshua nchini Marekani iko palepale lakini nimekubali ombi lao la kwenda kupigana nchini England nasubiri ofa yao'', aliandika Wilder kwenye Twitter.

Kwa upande wa meneja wa Joshua, Eddie Hearn, amesema atawatumia mkataba uongozi wa Wilder ili aone kama kweli wapo tayari au wanaongea tu kwenye mitandao."Tumeshangaa kakubali kuja kwetu kupigana sasa tutaweka mezani kila kitu kama watakubali masharti pambano litakuwepo'', alisema Eddie.

Kwenye pambano hilo Joshua mwenye miaka 28 ataweka mezani mikanda yake mitatu ya WBA, IBF na WBO huku Wilder mwenye miaka 32 ataweka mkanda wake wa WBC. Mshindi wa pambano hilo atakuwa bondia wa kwanza duniani kushikilia mikanda yote ya uzito wa juu.

Hata hivyo Joshua anaweza kupigana kwanza na Bondia kutoka Urusi Alexander Povetkin, ambaye anawania mkanda wa WBA na imeelezwa pande hizo mbili ziko mbioni kufikia makubaliano ya pambano hilo. Lakini pambano hilo linaweza kupisha la Joshua na Wilder endapo Povetkin atakubali kupigana na mshindi kati yao.