Jumatatu , 16th Jul , 2018

Mabingwa wa soka wa Italia klabu ya Juventus imekamilisha rasmi usajili wa mchezaji bora wa dunia, Cristiano Ronaldo kutokea Real Madrid baada ya kufuzu vipimo vya afya vilivyofanyika leo makao makuu ya klabu mjini Turin.

Cristiano Ronaldo wakati akifanyiwa vipimo vya afya.

Ronaldo mwenye miaka 33, amesaini mkataba wa miaka minne baada ya kukamilisha vipimo vya afya na atatambulishwa kwenye uwanja wa Juventus maarufu kama Allianz baadae jioni. Juventus sasa itailipa Real Madrid kiasi cha £105 milioni ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 317.

Katika maisha yake ya soka la ushindani, Ronaldo atakuwa anaanza maisha mapya kwa mara ya tatu baada ya ile ya kwanza akitoka Sporting CP ya nyumbani kwao Ureno ambayo aliichezea katika miaka ya 2002 na 2003 na kutua Manchester United.

Baada ya kuichezea Manchesteer United kwa miaka 6 Ronaldo aliamua kwenda kuanza maisha mapya kwenye klabu ya Real Madrid ya Hispania mwaka  2009, ambayo ameichezea kwa miaka 9 na sasa anaanza maisha mapya ndani ya Juventus.

Ripoti kutoka vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa tayari bodi ya wakurugenzi ya Juventus imeshapitisha wazo la kujenga sanamu ya Ronaldo nje ya uwanja wa Allianz lakini bado haijalipeleka kwa wawakilishi wa mashabiki ili nao watoe mtazamo wao.