Kagera yatangaza vita dhidi ya Azam

Thursday , 14th Sep , 2017

Ligi kuu ya soka Tanzania bara inataraji kuendelea kesho Ijumaa Septemba 15 kwa mchezo mmoja kupigwa kwenye uwanja wa Azam Complex ambapo wenyeji Azam FC wataialika Kagera Sugar.

Baadhi ya wachezaji wa timu ya Kagera Sugar.

Kuelekea mchezo huo kocha wa Kagera Sugar Meck Mexime amesema kikosi chake tayari kipo Dar es salaam tangu Jumatano. "Tayari tupo Dar es salaam na tumeshajiandaa toka Bukoba na tumefanya mazoezi mepesi jana leo tunapumzika kwaajili ya mechi kesho"' amesema Mexime.

Kwa upande wa majeruhi Mexime amethibitisha kuwa kikosi kina majeruhi watatu ambao ni Mohhamed Faki aliyevunjika mkono, George Kavila na Jaffar. Mtalaam huyo wa ufundi amesema wanamatumaini makubwa ya kupata ushindi kwani wamesafiri kutoka mbali kwaajili ya kuzisaka alama tatu.

Kagera Sugar ina alama 1 ikiwa katika nafasi ya 13 baada ya kutoka sare mchezo mmoja na kupoteza mmoja huku Azam FC wakiwa na alama 4 baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoa sare moja.