"Kama tuliwababua wababe wao, Yanga je? " - Masau

Jumanne , 14th Mei , 2019

"Kama tuliwababua wababe wao, Yanga tutawafanyaje" - Masau BwireAfisa habari wa klabu ya Ruvu Shooting, Masau Bwire ameendeleza tambo zake dhidi ya vilabu vikubwa nchini, ambapo safari hii ameivaa Yanga kuelekea mchezo wao wa ligi hii leo.

Masau Bwire

Ruvu Shooting itakuwa nyumbani jioni ya leo kupambana na Yanga katika wanja wa Uhuru, na Masau Bwire ameahidi kuwa hawatocheka mbele ya Yanga kwakuwa wanachokihitaji ni pointi tatu.

"Lengo letu kwenye michezo hii iliyosalia ni kukusanya pointi tatu tatu, tulianza kusema hili tangu tukiwa wa 19 wakati tuna mechi tano mkononi", amesema Masau.

"Sisi tunahitaji pointi tatu kutoka kwao, sasa kama tuliweza kuwababua wababe wao, hao (Yanga) ambao tunakwenda kukutana nao tutawafanyaje?, wakubali na wajipange kisaikolojia", ameongeza.

Yanga iko katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 80 na endapo itashinda mchezo wake wa leo dhidi ya Ruvu Shooting, itakwea kileleni kwa pointi 83 na michezo 36 ambayo itakuwa imekwisha cheza. Ruvu Shooting yenyewe iko katika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 42 katika michezo 35.

Rekodi inaonesha katika michezo mitano ya karibuni ya Ligi Kuu Tanzania Bara tangu msimu wa 2016/17, Yanga imefanikiwa kuibuka na ushindi katika michezo yote. Mchezo wa mwisho wa msimu huu, Desemba 2018, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-2.