Kauli ya Yanga baada ya kuwasimamisha viongozi

Jumapili , 29th Mar , 2020

Uongozi wa klabu ya Yanga umezungumza kufuatia barua rasmi ya kuwasimamisha baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji iliyotolewa Machi 27, 2020.

Makao Makuu ya Yanga

Kupitia kwa Afisa Habari wake, Hassan Bumbuli, Yanga imesema kuwa ni kweli kilichotokea kimeiathiri klabu na itatikisika lakini kila kitu kitakuwa sawa.

"Huu ni mtikisiko lakini ni kawaida kwa timu ya Wananchi kutokea kila kitu kitakuwa sawa na mipango inaendelea", amesema Bumbuli.

"Nadhani barua rasmi ilishatolewa na Kamati ya Utendaji, kwangu imepitia ili kuwafahamisha wanachama na mashabiki, kuhusu maelezo ya kwanini wamesimamishwa na kilichozandikwa kwenye barua ya majibu kwa GSM kamati ndiyo inafahamu", ameongeza.

Yanga iliwasimamisha viongozi wawili ndani ya klabu hiyo ambao ni Salim Rupia na Frank Kamugisha pamoja na kuridhia kujkiuzulu kwa wajumbe watatu ambao ni Rogers Gumbo, Shija Richard na Said Kambi.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Utendaji ya Yanga iliandika barua ya majibu kwa kampuni ya GSM ambao ni wadhamini wa klabu hiyo, kufuatia kujitoa kuisaidia klabu kwenye masuala mbalimbali nje ya makubaliano ya kimkataba ikilalamikia kuwa baadhi ya viongozi wa klabu hawaridhishwi na jinsi wanavyofanya kazi za kiuongozi.