Jumatatu , 15th Oct , 2018

Ushindi wa timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ wa mabao 3-0 dhidi ya Ethiopia umewapa furaha mashabiki wa nchi hiyo na kuamsha matumaini ya kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika AFCON 2019 nchini Cameroon.

Licha ya furaha na matumaini hayo kwa wakenya, ushindi huo una maana kubwa kwa mashabiki na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayotarajia kushuka dimbani hapo kesho dhidi ya Cape Verde katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.

Tukirejea nyuma katika mchezo wa kwanza uliofanyika nchini Ethiopia ambao uliisha kwa wenyeji Ethiopia kutoka sare ya bila kufungana na Kenya, ilishuhudiwa uwanja ukitapika kwa mashabiki ambao waliishangilia timu yao kwa nguvu kiasi cha kuwashangaza Harambee Stars.

Hali hiyo ilipelekea baada ya kumalizika kwa mchezo huo, nahodha wa timu ya Kenya, Victor Wanyama kutamka wazi kuwa hakuwahi kuona hata siku moja viwanja vya Afrika vikifurika watu namna ile na kuliomba shirikisho la soka nchini kwake kuweka mazingira ya kujaza uwanja ili walipize kisasi.

Shirikisho la soka la Kenya (FKF) likakubali ombi hilo na kuruhuhusu mashabiki kuingia bure uwanjani ili kuishangilia kwa nguvu timu yao kulikopelekea Harambee Stars kuibuka na ushindi wa mabao hayo matatu. Matukio hayo yote yanaipa funzo kubwa Taifa Stars na mashabiki wake namna gani wanavyotakiwa kuipigania timu yao huku shirikisho la soka nchini (TFF) likitengeneza mazingira ya kupatikana kwa mafanikio hayo.

Taifa Stars na mashabiki wake wanatakiwa wajue thamani ya timu ya taifa, kila mmoja atakayeingia uwanjani kesho ajue kuwa ana mzigo wa kuchangia mafanikio ya timu yake. Nafasi ya mchezo wa kesho ni ya dhahabu kwani ikichezewa inaweza kuuwa ndoto za Tanzania kucheza AFCON ambay ilishiriki mara ya mwisho mwaka 1980 nchini Nigeria.