Jumamosi , 8th Aug , 2020

Nyota wa zamani wa vilabu vya Yanga na Simba, Bakari Malima ''Jembe Ulaya'' ameweka wazi kwamba wachezaji Shiza Kichuya, Ibrahim Ajibu( wote kutoka Simba na Abdallah Shaibu ''Ninja'' (Kutoka Yanga) walikosea kurudi nyuma liha ya kupata nafasi ya kucheza soka nje ya nchi.

Nyota wa Klabu ya Simba, Ibrahim Ajibu (Pichani) akiwa anapokea maelekezo ya Kocha wake Sven Vandenbroeck katika moja ya mchezo.

Akizungumza na Kipindi cha Michezo cha Kipenga kinachoruka kila siku za Jumatatu mpaka Ijumaa saa 2- 3 Usiku, Jembe Ulaya ambaye alitamba enzi zake miaka ya 1996 hadi 2004 katika vilabu vyote kongwe nchini, amesema mchezaji kama Kichuya alienda Misri, alipaswa kupambana hata kama mazingira hayakua mazuri lakini Taifa hilo ni bora upande wa soka na angeonekana kupitia kipaji chake.

Kwa upande wa Ajibu vilevile alifanya makosa makubwa alipoikataa ofa ya kujiunga na TP Mazembe ya Congo iliyotumwa wakati akimaliza msimu uliopita akiwa na Yanga, kwani anaamini klabu hiyo yenye tabia za kushiriki mara kwa mara kwenye michuano ya kimataifa ya Afrika, angepata uzoefu na kujifunza mengi kama ilivyokua kwa Mbwana Samatta ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa nchini Uingereza.

Aidha Malima ameongeza pia alishangazwa na mchezaji Abdallah Shaibu kurejea nchini na kujiunga na timu yake ya zamani ya Yanga, kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kurejea nyuma kwa hatua nyingi, huku akiamini kwamba mazingira na ufalme wanaopewa wachezaji hao hapa nchini hawapewi huko ugenini.

Mchezaji huyo aliyekua na uwezo wa kucheza nafasi za ulinzi na kiungo, amewataka wachezaji wa Tanzania kujifunza kuwa wavumilivu kwa kuwa Tanzania na Mataifa ya wenzetu yana mazingira tofauti, na wanahitaji kupigania kipaji chao ili wapate majina huko kama ilivyokua kwa Samatta alipokwenda nchini Congo, hakufanikiwa ndani ya msimu mmoja au miwili pekee.

Hata hivyo amewashauri Kichuya na Ajibu kukubali kujiunga na Timu nyingine kwa mkopo ili wakapate nafasi ya kucheza mara kwa mara ,kwani kuendelea kukaa benchi Simba kutawapunguzia morali ya kupambana.

Kwa upande wa Ninja ,amemtaka kuendelea kuamini kwamba anahitaji kwenda nje ya nchi, hivyo acheze kwa malengo ndani ya Yanga ili aende nje ya nchi.