Kilichoishusha Lipuli daraja chafahamika

Jumamosi , 1st Aug , 2020

Kocha wa Lipuli Fc ya Iringa ,Nzeyimana Mailo amesikitishwa na Uongozi wa timu hiyo kushindwa kumlipa malimbikizo ya mshahara wake tangu Mwezi Februari licha ya kumaliza msimu na timu hiyo.

Kikosi cha Lipuli Fc ya Iringa ambayo imeshuka daraja.

Mailo Raia wa Burundi amesema kibaya zaidi kuna fedha zake ambalo aliwaomba wamtunzie lakini ilipofika muda wa yeye kuondoka, hawakumuwekea kwenye akaunti yake na waliishia kumpa nauli pekee ya kurejea nyumbani kwake bila ya posho ya kurudi nayo nyumbani kwake.

Vile vile kocha huyo ameongeza kuwa si yeye pekeyake bali hata wachezaji walipewa nauli tu kiasi cha shilingi 5000 jambo ambalo anaamini ni fedheha kwa klabu, na hata kushuka kwa timu kulichangiwa na matatizo kama hayo kwa wachezaji.

Aidha kocha huyo amesema alikua na mkataba hadi Mwezi Januari Mwakani lakini kwa kuwa hajalipwa mshahara kwa miezi mitatu, hana haja ya kuutumikia uliosalia kwa kuwa inawezekana watagombana zaidi na viongozi wa timu hiyo.

Hata hivyo Mailo amesema hatoishitaki kabu hiyo katika Shirikisho la soka Duniani FIFA ,kwani anapenda amani, ingawa amelitaka Shirikisho la soka nchini kufuatilia changamoto za uongozi wa vilabu vyake ambayo kwa asilimia kubwa vinawapa shida kubwa makocha na wachezaji.

Lipuli ilishuka daraja baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga,na sasa itashiriki ligi daraja la kwanza msimu ujao.